Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kufuatia vitisho vya mara kwa mara vya Marekani kuhusu uwezekano wa kushambulia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia kutoa matusi dhidi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, Baraza la Wanazuoni wa Palestina nchini Lebanon na nje ya nchi hiyo lilitoa taarifa rasmi, huku likitangaza uungaji wake mkono kwa taifa na mfumo wa Iran, na kulaani vikali vitisho hivyo pamoja na kuikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kunyamaza kimya mbele ya vitendo hivyo vya uchochezi.
Tarjama kamili ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:
Sote tumesimama pamoja nanyi na pamoja na Iran ya heshima na utu — mlinzi wa Palestina na wanyonge wote. Tunampongeza kiongozi na taifa lenu kwa maadhimisho ya miaka arobaini na saba ya ushindi wa Mapinduzi yenu makubwa, na tunalaani vikali vitisho vya Marekani dhidi ya Ayatullah Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde) na dhidi ya Iran na eneo zima.
Tunarudia kusisitiza kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; nchi ambayo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, kwa subira na uaminifu, kwa kutetea haki na Palestina, na kwa kulinda heshima, utu, dini, mustakabali, umoja na utamaduni wa vizazi vijavyo vya Umma wa Kiislamu, itawashinda maadui zake.
Pia tunalaani vikali vitisho vya Marekani dhidi ya uongozi na nchi yenu, na tunaushutumu ukimya kamili wa jumuiya ya kimataifa, Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa mbele ya vitisho hivyo dhidi ya nchi yenu pendwa.
Tukitahadharisha juu ya hatari ya hatua hii, tunakumbusha kuwa; ni wajibu kwa wote kuwa macho na kufahamu kwamba ikiwa vita hii ya uchokozi dhidi ya Iran itatokea, itakuwa vita ya hatima — vita ya “kuwepo au kutokuwepo” ambayo itaamua mustakabali wa eneo hili na vizazi vyetu vijavyo kwa miaka mingi.
Baraza la Wanazuoni wa Palestina linatoa wito kwa wote kuunganisha safu zao, kuiunga mkono Iran na kuwa pamoja nayo, kwa sababu Iran ya leo ni mstari wa kwanza wa ulinzi wa heshima ya Umma na mustakabali wa eneo zima.
Na mwishoni tunawaambia: hakika haki itashinda, na Iran kwa uimara wake na mapambano yake dhidi ya adui Mzayuni-Mmarekani ni mwakilishi wa haki, dini na Uislamu. Na batili, ambayo alama yake ni shetani, adui Mzayuni, Marekani, Magharibi dhalimu na Waarabu waoga waliokata tamaa ya heshima na utu wao na kuiacha Ghaza iwe mahali pa kuchinjwa, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu itavunjwa.
Baraza la Wanazuoni wa Palestina nchini Lebanon na nje yake

Maoni yako